TMA YATOA UTABIRI WA MSIMU WA MVUA ZA MASIKA 2024 KWA MAENEO YANAYOPATA MVUA MARA MBILI KWA MWAKA.

Dar es Salaam; Tarehe 22, Februari 2024.

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa rasmi utabiri wa msimu wa mvua za Masika 2024 kwa maeneo yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka. Akizungumza wakati wa mkutano na vyombo vya habari katika ukumbi wa Ubungo Plaza, tarehe 22/02/2024, Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TMA na Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Kimataifa la Sayansi ya Mabadiliko ya hali ya hewa, Dkt. Ladislaus Chang’a alisema maeneo mengi ya nchi yanayopata misimu miwili ya mvua yanatarajiwa kupata mvua za wastani hadi juu ya wastani.

“Mvua za wastani hadi juu ya wastani zinatarajiwa katika maeneo mengi ya nchi, Mvua hizi zinatarajiwa kuanza wiki ya nne ya mwezi Februari katika maeneo mengi na kuisha wiki ya tatu na ya nne ya mwezi Mei 2024, Aidha, aliongeza kuwa ongezeko la mvua linatarajiwa katika kipindi cha mwezi Machi 2024.” Alisema Dkt. Chang’a.

Akizungumzia athari zinazoweza kujitokeza, Dkt. Chang’a alisema vipindi vifupi vya mvua kubwa vinaweza kujitokeza hivyo kuweza kusababisha mafuriko, milipuko ya magonjwa pamoja na athari nyingine zitokanazo na mvua nyingi.

Katika hatua nyingine, Dkt. Chang’a alimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuboresha miundombinu ya uangazi wa hali ya hewa na hivyo kuiwezesha TMA kufikia hatua ya kuongeza usahihi wa utabiri.

Dkt. Chang’a alisisitiza jamii kuendelea kufuatilia taarifa za mara kwa mara zinazotolewa na TMA kwa vile ni za uhakika, huku akibainisha kuwa usahihi wa msimu wa Vuli 2023 ulikuwa asilimia 98.

Kwa taarifa zaidi tembelea; https://www.meteo.go.tz/uploads/publications/sw1708594104-Mwelekeo%20wa%20Mvua%20za%20Masika%202024.pdf

Related Posts